WIZARA YA UJENZI YAWASILISHA KWA KAMATI TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA WA FEDHA 2024/25
Dodoma

Wizara ya Ujenzi imewasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na makadirio ya Mpango na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/26 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu leo tarehe 20 Machi, 2025 jijini Dodoma.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ameeleza kuwa Wizara kupitia taasisi zake imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara ya Mzunguko wa Nje ya Dodoma, ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi na barabara zake unganishi, ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Kasi (Awamu ya Tatu na Nne).
Vilevile, Wizara inaendelea na ujenzi wa barabara ya Mkange – Tungamaa – Pangani (km 170.8), Daraja la Pangani (m 525) pamoja na ujenzi wa madaraja mengine katika maeneo mbalimbali yapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Ameongeza kuwa sambamba na miradi ya barabara inayoendelea katika mikoa mbalimbali pia inaendelea na utekelezaji wa miradi ya viwanja vya ndege, ujenzi wa nyumba za watumishi na majengo ya Serikali, vivuko vipya sita pamoja na maegesho yake na ukarabati wa vivuko vya MV Kilombero II, MV Nyerere, MV Ukara I, MV Kigamboni na Magogoni.
Ulega ameeleza kuwa Wizara imejipanga kutekeleza miradi muhimu ikiwa ni azma ya kutimiza malengo ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan sambamba na kukamilisha miradi ambayo imeainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020.





Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000