WAZIRI KOMBO; HATMA YA MAENDELEO AFRIKA INATEGEMEA ZAIDI UMOJA WETU

Uturuki

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) ameeleza kuwa hatma ya maendeleo ya kiuchumi Barani Afrika inategemea umoja ulio imara wa bara hilo. 

Waziri Kombo ameeleza hayo alipochangia mjadala kuhusu “Kukua kwa Nafasi ya Afrika katika Siasa za Dunia” (The Rising Role of Africa in World Politics”) kwenye Mkutano wa 4 wa Diplomasia wa Antalya (Antalya Diplomacy Forum – ADF2025) uliofanyika Aprili 12, 2025 nchini Uturuki. 

Akitoa mchango wake katika mjadala huo Mhe. Waziri Kombo ameeleza kuwa Afrika inahitaji kuwa na umoja thabiti utakaowezesha kujenga utamaduni wa kujadili kwa kina na uwazi masuala ya msingi ya maendeleo ili kupata ufumbuzi wa changamoto za kiuchumi zinazolikabili bara hilo kwa sasa. 

Mbali na kuhimiza umoja, Mhe. Waziri Kombo ametoa mapendekezo kadhaa ya kuzingatiwa barani Afrika ili kujenga mazingira rafiki yatakayowezesha ukuaji wa Uchumi yakiwemo maboresho ya mfumo wa elimu ambayo yatawawezesha vijana kujitegemea, kwa kutambua uwingi na thamani ya rasilimali zilizopo ili ziweze kutoa mchango chanya kwenye maendeleo ya uchumi. 

Mapendekezo mengine yaliyotelewa katika mjadala huo ni kuhakikisha kuwa Serikali zinakuwa na mfumo mzuri wa ushirikishwaji wa makundi maalumu ikiwemo vijana na wanawake katika hatua za kufanya maamuzi yanoyohusu matumizi ya rasilimali ili kuepuka migogoro na ubadhilifu. 

Viongozi wengine waliokuwa katika mjadala huo ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Ivory Coast Mhe. Léon Kacou Adom, Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji Mhe. Maria Manuela Dos Santos Lucas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana Mhe. Samuel Okudzeto Ablakwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Liberia Mhe. Sara Beysolow Nyanti, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Mhe. Olivier Jean Patrick Nduhungirehe, Waziri wa Mambo ya Nje wa Benin Mhe. Olushegun Adjadi Bakari, na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Ulinzi cha Uturuki Prof. Mehmet Özkan.

Mkutano wa 4 wa Diplomasia wa Antalya ulifunguliwa rasmi tarehe 11 Aprili , 2025 na Rais wa Uturuki Mheshimiwa Recep Tayyip Erdoğan, ambapo ulihudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali, Mawaziri Wakuu, Mawaziri wa Mambo ya Nje, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa, watunga sera, wafanyabiashara, wanataaluma, na wawakilishi wa asasi za kiraia kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000