WAKAGUZI WASAIDIZI WA MADINI PAMOJA NA WASIMAMIZI WA MADINI UJENZI NA VIWANDANI WAFUNDWA
Dodoma

WASIMAMIZI wa madini ujenzi pamoja na wakaguzi wasaidizi wa madini wametakiwa kufanya kazi kwa ufanisi na kuhakikisha wanafuata taratibu na sheria za nchi katika utoaji wa huduma.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Hamisi Kamando katika kikao kazi kilichowakutanisha Wasimamizi wa Madini Ujenzi na Viwanda, Wakaguzi Wasaidizi wa Madini (AMAs) pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Tume ya Madini .
Kupitia hotuba hiyo amesema kikao hicho kitasaidia kujenga uelewa wa pamoja kuhusu majukumu, changamoto pamoja na mbinu mbalimbali zinazotumika katika ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na madini ujenzi na viwanda ambayo yatapelekea kufikia lengo la makusanyo ya Tume.

Amewapongeza kwa kuendelea kujitoa kwao katika usimamizi wa shughuli za madini hususani katika sekta ndogo ya madini ujenzi na viwanda, kwa kuwa tangu kuanzishwa kwa Tume mchango wa madini ya viwandani unazidi kupanda kila mwaka kutoka Shilingi Bilioni 17.6 mwaka 2018/2019 hadi kufikia Shilingi Bilioni 33.0 mwaka 2023/2024.
Amesema kwa kutambua mchango wa watumishi hao Tume ya madini inaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa kuhakikisha vitendea kazi vinapatikana kwa wakati kwa lengo la kuongeza ufanisi na kazi .
Itakumbukwa mnamo mwezi Oktoba, 2024 Waziri wa Madini, Mhe Anthony Peter Mavunde (Mb) aligawa magari 25 ,pia usambazaji wa pikipiki 40 katika ofisi mbalimbali za mikoa ili kuboresha utendaji kazi na kuongeza ukusanyaji wa Maduhuli .
Aidha Tume ya madini kwa sasa inaenda na mfumo wa kielektroniki wa POS ili kurahisisha utendaji kazi.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000