UDUMAVU KWA WATOTO WENYE UMRI CHINI YA MIAKA MITANO BADO NI TATIZO – DUGANGE.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Afya Mhe. Festo Dugange amesema takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano bado ni kikubwa ambapo kwa mkoa wa Kigoma ni 27.1%, Katavi 32.2%, Njombe50.4%, Songwe 31.9% na Rukwa 49.8%.

Amesema hayo katika hafla ya kusaini hati za makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa lishe unaofadhiliwa na shirika la USAID iliyofanika leo Mei 7, 2024 katika ukumbi wa Sokoine Jijini Dodoma.

Dugange amesema viwango vya matatizo ya lishe nchini vimeendelea kupungua mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2022 kiwango cha udumavu nchini ni 30% ikilinganishwa na 34% mwaka 2015.

Aidha, Mhe. Dugange amesema tunapaswa kuendelea kuhamasisha ulaji wa chakula mchanganyiko chenye virutubisho na kuzingatia mtindo bora wa maisha.

“tuweke kipaumbele katika kuimarisha usafi wa mazingira na kutokomeza Imani na mila potofu zinazoathiri lishe”amesema Mhe. Dugange

Mhe.Dugange amewataka viongozi katika Mikoa na Halmashauri kuzingatia na kudhibiti maradhi yanayochangia matatizo ya lishe na kuimarisha uhakika wa chakula na matunzo bora ya wanawake na watoto.

“Tukiyafanya haya yote kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu program hii ya lishe inayozinduliwa leo itachangia kikamilifu na kuongeza kasi ya kupunguza udumavu na matatizo mengine ya lishe nchini” amesema Mhe. Dugange

Mhe.Dugange ameahidi kuwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI itatoa ushirikiano wa kutosha kwa wadau wote wa program ya lishe ili kuhakikisha kuwa malengo ya program hii yanafikiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa ujumla.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000