SERIKALI YATOA LESENI KUBWA YA UCHIMBAJI MADINI YA KINYWE KWA EcoGraph
Tanzania

• Mradi wa Epanko Graphite Kuinufaisha Tanzania Kibiashara, Kiuchumi
• Kuchangia Zaidi ya Shilingi Trilioni 5 kwenye Pato la Taifa
• Tanzania kuwa Kiungo Muhimu Katika Sekta ya Nishati Safi Duniani
Tanzania imeandika historia mpya katika Sekta ya Madini baada ya Machi 3, 2025, Serikali kutoa Leseni Kubwa ya Uchimbaji (Special Mining Lisence- SML) wa Madini ya Kinywe (Graphite) kwa Kampuni ya EcoGraf Limited kupitia Mgodi wa Epanko Graphite, uliopo Kijiji cha Epanko Wilaya ya Mahenge, Mkoani Morogoro.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa Serikali wa kuboresha Sekta ya Madini hapa nchini sambamba na kuongeza thamani kwa maliasili zake ikiwemo za madini ambako Mradi huo unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika uchumi, viwanda, ajira, na nafasi ya Tanzania katika soko la kimataifa la nishati safi.
Katika taarifa yake kwa umma, Mkurugenzi Mtendaji wa EcoGraf, Andrew Spinks amesema kuwa Serikali ya Tanzania ilifanya tathmini ya kina ya maendeleo ya Mradi wa Epanko na kwamba Kampuni hiyo inatoa shukraniza dhati kwa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, kwa msaada wao na kwa kuidhinisha utolewaji wa leseni hiyo.
Mapato Makubwa kwa Serikali na Uwekezaji Endelevu

Serikali ya Tanzania itanufaika na kodi na tozo mbalimbali zitakazotokana na shughuli za mgodi wa Epanko. Mapato hayo yanaweza kuelekezwa katika miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa shule, hospitali, barabara, na miradi mingine ya kijamii.
Licha ya dola milioni 850 sawa na shilingi trilioni 2.1 zinazotarajiwa kulipwa na kampuni hiyo kama kodi, gawio, ada, mrabaha na ununuzi wa huduma na bidhaa tofauti katika kipindi cha kuendesha shughuli zake, inakadiriwa itachangia zaidi ya dola bilioni 2.5 sawa na shilingi trilioni 5.6 kwenye pato la Taifa (GDP).
Mapinduzi ya Sekta ya Viwanda na Ongezeko la Thamani kwa Madini Kinywe (Graphite)
“Hatua hii inafanya Mradi wa Epanko kuwa mradi mkubwa zaidi ya madini kinywe barani Afrika ambao upo tayari kuendelezwa. Akiba ya madini kinywe ya Epanko (Ore Reserve) inakadiriwa kuwa tani 290.8 Mt, ikitoa uhakika mkubwa katika uendelezaji wa madini, ubora wa madini yatakayosafishwa, mambo ambayo ni muhimu katika kuamua bei sokoni” imesema taarifa hiyo.
Epanko Graphite itahakikisha kwamba uchakataji wake unafanyika hapa nchini kabla ya kusafirishwa nje huku Tanzania ikijitengenezea nafasi ya kuwa kitovu cha uzalishaji wa madini hayo yenye thamani ya juu, ambayo ni malighafi muhimu kwa utengenezaji wa betri za magari ya umeme na mifumo ya kuhifadhi nishati mbadala.
“Utolewaji wa Leseni Kubwa ya Uchimbaji (SML) ni hatua muhimu katika maendeleo ya Epanko na sharti kuu kwa mchakato wa ufadhili, ambao utasaidia hatua ya kwanza ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha kuchenjua grafiti chenye uwezo wa kuzalisha tani 73,000 kwa mwaka.” Imeongeza taarifa hiyo.
Tanzania kuwa Kiungo Muhimu Katika Sekta ya Nishati Safi Duniani

Dunia inashuhudia mageuzi makubwa ya kuachana na nishati ya mafuta na kuelekea kwenye nishati safi. Magari ya umeme na mifumo ya kuhifadhi nishati ya jua na upepo vinahitaji betri bora zenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi chaji kwa muda mrefu. Madini ya Kinywe (Graphite) ni moja ya malighafi muhimu zaidi katika utengenezaji wa betri hizo, na mradi wa Epanko utaiweka Tanzania katika nafasi ya kimkakati kama mtoa huduma wa malighafi hii kwa masoko ya makubwa ya Ulaya, Asia, na Amerika Kaskazini.
Kwa kuzingatia kuwa Madini ya Kinywe ya Tanzania ni ya kiwango cha juu, nchi inaweza kuwa moja ya wazalishaji wakubwa duniani, hivyo kuongeza nguvu ya Tanzania katika soko la kimataifa la betri za umeme. Ndani ya kipindi kifupi inaweza kuongeza nafasi ya Tanzania katika diplomasia ya kiuchumi, kwani nchi zilizoendelea zinauhitaji mkubwa wa malighafi hiyo.
Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000