TUTUNZE MIRADI YA MAENDELEO KAMA TUNAVYOTUNZA MACHO YETU: RAIS .DKT SAMIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wa Kizimkazi na maeneo jirani kutunza na kulinda miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, akisisitiza kuwa miradi hiyo ni msingi wa uchumi na ustawi wa wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Agosti 13, 2026, Zanzibar, mara baada ya kuzindua Mradi wa Maji Kizimkazi, ambapo amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali kupitia miradi mbalimbali unapaswa kulindwa ili iendelee kutoa huduma na manufaa yaliyokusudiwa kwa muda mrefu.

“Ni wajibu na ni lazima tutunze miradi hii kama tunavyotunza macho yetu. Miradi hii ni fursa zetu, ni uchumi na ustawi wa maisha yetu,” amesema Rais Samia.

Amesema mafanikio ya utekelezaji wa miradi hiyo yanatokana kwa kiasi kikubwa na uwepo wa amani nchini, hivyo amewataka wananchi kuendelea kuitunza amani ili Serikali iweze kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha maisha yao.

“Miradi hii tumeweka kuileta kwa sababu nchi yetu ina amani. Niombe sana ndugu zangu tuendelee kutunza amani yetu ili tupate maendeleo zaidi,” amesema.

Rais Samia pia amesema kaulimbiu ya “Mapinduzi Daima” inapaswa kuendelea kuakisi mapinduzi katika maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi, akieleza kuwa Mapinduzi yalishafanyika na jukumu la sasa ni kuhakikisha mafanikio hayo yanaendelezwa kupitia maendeleo endelevu.

“Tunaposema Mapinduzi Daima, Mapinduzi ya sasa ni maendeleo,” amesema.

Akizungumzia Mradi wa Maji Kizimkazi, Rais Samia amesema mradi huo umejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa pamoja na ongezeko la watu na ukuaji wa miji, huku uwezo wake ukiwekwa karibu mara mbili ya mahitaji ya sasa ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji hata katika miaka ijayo.

Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuupenda, kuutunza na kuilinda miundombinu ya mradi huo kwa kuwa fedha nyingi zimetumika katika utekelezaji wake, hivyo uharibifu au matumizi yasiyo sahihi yanaweza kupunguza au kudhoofisha manufaa yanayotarajiwa.

Rais Samia amesema utunzaji wa miradi ya maendeleo ni jukumu la pamoja kati ya Serikali na wananchi, akisisitiza kuwa kulinda miundombinu hiyo ni kulinda uwekezaji unaolenga kuboresha maisha ya wananchi na kuhakikisha huduma hizo zinaendelea kunufaisha jamii kwa sasa na vizazi vijavyo.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000