KIGOMA KUWA KITOVU CHA FURSA ZA BIASHARA BAADA YA UJENZI WA SGR TABORA–KIGOMA : RAIS SAMIA ABAINISHA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kuwa kituo kikubwa cha biashara barani Afrika kutokana na rasilimali na fursa ilizonazo.
Ameyasema hayo Julai 20, 2026 mkoani Kigoma wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) Tabora–Kigoma na uzinduzi wa meli nne za mizigo katika Bandari ya Kigoma.
Amesema kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira bora kisera na kisheria pamoja na kujenga miundombinu ya kimkakati ili kukuza biashara, uwekezaji, ajira na ustawi wa wananchi.
Aidha mheshimiwa Rais amebainisha kuwa Kigoma haitabaki tena kuwa mwisho wa reli kama ilivyokuwa ikifahamika hapo awali, bali itakuwa mwanzo wa kufunguka kwa fursa za kibiashara na uwekezaji kutokana na miundombinu inayojengwa kuunganisha mkoa huo na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Ameongeza kuwa mradi wa SGR Tabora–Kigoma wenye urefu wa takribani kilometa 506 unagharimu dola za Marekani bilioni 2.74, sawa na Shilingi trilioni 7.4, na utakapokamilika utaunganisha Kigoma na mikoa ya Tabora, Dodoma, Morogoro hadi Dar es Salaam pamoja na mtandao wa reli unaoelekea Mwanza.
Aidha, amebainisha kuwa kukamilika kwa reli hiyo kutawezesha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kufika Kigoma kwa haraka na kwa uhakika, jambo litakalopunguza muda na gharama za usafirishaji kwa wafanyabiashara na wajasiriamali.
Pia ameongeza kuwa SGR Tabora–Kigoma ni sehemu ya jitihada za kuimarisha nafasi ya Tanzania katika usafirishaji wa kikanda, huku Kigoma ikitarajiwa kunufaika kutokana na nafasi yake ya kimkakati inayoiunganisha Tanzania na nchi jirani.



Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000

