WAZIRI NDEJEMBI AKUTANA NA WANANCHI WA KATA YA NYATWALI, DODOMA 

Dodoma

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amekutana na wananchi wa Kata ya Nyatwali Wilayani Bunda Mkoa wa Mara Ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma ambapo wamejadili masuala mbalimbali kuhusu eneo hilo.

Majadiliano hayo yamefanyika Mei 22, 2025 katika Ofisi za Makao Makuu ya Wizara hiyo zilizopo katika Mtaa wa Ardhi katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

“Wananchi wameridhika na yale yaliyofanywa na serikali, kuna vipengele vya kufanyia kazi kwa haraka, kuna ardhi ya eka 980, kuna ardhi ya kikundi cha umwagiliaji, kuna eneo la Masaga na shamba la malisho. Tumekubaliana twende tukayafanyie kazi masuala yote kwa haraka” amesema Waziri Ndejembi.

Waziri Ndejembi amesema Wizara inayafanyia kazi masuala yaliyowasilishwa na wananchi hao ikiwemo kurasimisha ekari 980 za wananchi hao eneo hilo na kuongeza kuwa tayari serikali imeshalipa zaidi ya Sh. Bilioni 50 ikiwa ni fidia kwa wananchi wa Nyatwali.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nyatwali Halmashauri ya Bunda mkoani Mara Malongo Mashimo asema lengo la ziara yao ni kuishukuru Serikali kwa kuwapa huduma wananchi wa Nyatwali kwa kupata fidia zaidi ya asilimia 90 na kuongeza kuwa Waziri amesema suala lao litafanyiwa kazi haraka iwezekavyo kuaanzia sasa.

Naye Mwenyekiti wa UWT Kata ya Nyatwali Bi. Christina Masalu amesema wamefika Wizarani hapo wamepokelewa vizuri na viongozi wakiongozwa na Waziri Deogratius Ndejembi, Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga na Kamishna wa Ardhi Bw. Nathaniel Nhonge.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000