WAZIRI MKUU: WATOTO WAPELEKWE SHULE, MSIRUHUSU WAUZE MAANDAZI, KARANGA 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) amewataka wazazi wahakikishe wanawaandikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule badala ya kuwaacha wakauze maandazi, karanga na miwa.

Amewataka watendaji wa kata kote nchini wakae na watendaji wa vijiji na mitaa ili kuwahimiza suala la uandikishaji wa watoto wenye umri wa kwenda shule. “Mtoto wa Kitanzania anatakiwa kwenda shule, kwa sababu mtoto huyu leo ameandaliwa utaratibu wa kuanzia chekekea, shule za msingi hadi sekondari. Tunahitaji kuona watoto wa Busega wakienda shule wote,” amesisitiza.

“Niwasihi wazazi, fuatilieni mahudhurio ya watoto wenu ili kubaini kama kweli wanaenda shule na wanasoma. Wanaporudi nyumbani, kagueni madaftari yao ili kuona wamejifunza nini. Zaidi ya hayo, muwasimamie watoto wa kike ili wahitimu masomo yao bila kubughudhiwa,” amesisitiza. 

Ametoa wito huo leo (Jumapili, Desemba 22, 2024) wakati akizungumza na maelfu ya wajumbe waliohudhuria Mkutano Mkuu wa CCM wa Wilaya ya Busega, uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Lion of Judah, wilayani Busega, mkoani Simiyu. 

Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza sana kwenye upatikanaji wa elimu nchini kwa kutoa fedha ya ujenzi wa shule, madarasa na mabweni. “Pia ametoa fedha za elimu bila ada ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa ya elimu.”

Kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, Waziri Mkuu amesema umefika wakati sasa taasisi zenye watu zaidi ya 100 zianze kutumia nishati hiyo huku akiwakumbusha wadau kuwa ukomo wa matumizi ya nishati chafu ni Desemba 31, mwaka huu. 

“Wananchi mmoja waanze taratibu kuachana na matumizi ya nishati chafu kwa kubadilisha teknolojia. Tuhame kutoka kwenye kuni na mkaa na tuanze kutumia nishati ya gesi, umeme na aina nyingine ya mkaa ambao unatenegenezwa kwa kutumia takataka.”

Ametumia fursa hiyo kuwaelezea wajumbe wa mkutano huo, mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. “Fedha nyingi zimetolewa kwenye sekta ya elimu ambazo zimetumika kujenga miundombinu ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya kati (VETA) pamoja na ukarabati mkubwa wa vyuo vikuu.”

Kwenye sekta ya afya, Waziri Mkuu amesema zimetolewa fedha nyingi kujenga vituo vya afya, hospitali za wilaya na za halmashauri zenye hadhi ya hospitali za wilaya pamoja na ujenzi wa hospitali za kanda.

Kuhusu umeme, Waziri Mkuu amesema: “Vijiji vyote vya mkoa huo vimepata umeme, imebakia tu kazi ya wananchi kuuvuta. Leo hii tunaenda kwenye ngazi ya vitongoji na kupeleka umeme kwenye visiwa, iwe ni umeme wa jua au wa kupitisha kwenye bomba chini ya maji kwenda kwenye kisiwa kama cha Ukerewe.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema utulivu uliopo kwenye wilaya ya Busega unatokana na sera za CCM ambazo zinatabirika tangu enzi za waasisi wa Taifa hili. “Mshikamano na utulivu, uwepo wa maadili ni utamaduni wa Taifa letu na hata matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa yamedhihirisha imani waliyonayo wananchi kwa Chama cha Mapinduzi.”

Mapema, Mbunge wa Busega, Simon Songe kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma nyingi za kijamii kwenye wilaya hiyo ndani ya muda mfupi. “Watu wa Busega tuna imani sana na Serikali ya awamu ya sita, maendeleo yaliyofanyika ni makubwa ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa. Tuna imani kuwa itakamilika mapema ili wakazi wa Busega waweze kwenda Dar es Salaam chini ya saa sita,” amesema.

Ameishukuru Serikali kwa kutoa sh. bilioni 19.9 ambazo katika kipindi cha Desemba 2020 hadi Oktoba 2024, zimewezesha utekelezaji wa miradi kadhaa ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa vyumba vya madarasa, vyoo na madawati.

“Mradi wa VETA utakaogharimu shilingi bilioni 1.484 tayari umeshaanza kujengwa na ninaamini mwaka 2026 utakuwa umekamilika na wananchi wataanza kuitumia. Tunamshukuru sana Mhe. Rais na Serikali ya awamu ya sita kwa uwekezaji huu muhimu kwa maendeleo ya vijana wetu,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi alisema mkoa huo umepokea sh. bilioni 858.5 ambazo zimetumika kuboresha sekta za elimu, afya, maji na umeme.

Aliishukuru Serikali kwa kupeleka magari ya wagonjwa manne, mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria utakaogharimu sh. bilioni 440 na ujenzi wa kituo cha kupozea umeme kwa gharama ya sh. bilioni 97.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000