WAWEKEZAJI WAKARIBISHWA KAGERA
Kagera
Wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi wamekaribishwa kuwekeza mkoani Kagera kufuatia hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ambazo mkoa wa huo umefikia ikiwa ni pamoja na mipango ya maendeleo na fursa nyingi za uwekezaji zilizopo.
Mkoa wa Kagera ni wa pili kwa uzalishaji wa samaki na fursa ya uvuvi nchini ukitanguliwa na Mkoa wa Mwanza fursa ambayo inawanufaisha wakazi wake kwa kuwapatia ajira, lishe bora, kipato na maendeleo ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa makazi bora kutokana na shughuli za uvuvi.
Akizungumza Desemba 19, 2024 katika Uwanja wa Kaitaba wilayani Bukoba mkoani Kagera wakati aliposhiriki katika Tamasha la Pili la Uwekezaji la mkoa huo ikiwa sehemu ya Wiki ya Tamasha la Ijuka Omuka (Kumbuka Nyumbani), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani mazao ya uvuvi, viwanda vya kutengeneza zana za uvuvi kama nyavu, kamba, vifaa vya kujiokolea na mashine za boti badala ya kuagiza vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.
Dkt. Biteko amesema kuwa Mkoa wa Kagera unaongoza kitaifa kuwa na ranchi 6 za mifugo kati ya ranchi 15 zilizopo nchini. Ametaja ranchi hizo kuwa ni Missenyi, Mabale, Kikulula, Mwisa II, Kitengule na Kagoma.
Ameendelea kusema kuwa mkoa huo kupitia halmashauri zake zote umetenga jumla ya hekta 345,430.97 kwa ajili ya malisho ya mifugo ambapo uwepo wa maeneo hayo ya malisho na ufugaji yanatoa fursa kubwa ya uwekezaji kwa kuanzisha ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa nyama na maziwa ili kuvutia uanzishwaji wa viwanda vya kuchataka nyama na maziwa hasa katika maeneo yenye ranchi za Taifa.
“ Naiona Kagera inakwenda kukua kwa kasi kubwa sana na nitumie fursa hii kuwaomba na kuwaalika wawekezaji kote nchini na nje ya nchi kuja kuwekeza Kagera kutokana na fursa zilizopo kwani mazingira ya uwekezaji ni mazuri na uongozi wa mkoa umejipanga vyema kuwapokea na kuwahudumia kwa viwango,” amesema Dkt. Biteko
Ameongeza kuwa Mkoa wa Kagera pia unaongoza kwa uzalishaji wa zao la ndizi kwa wastani wa tani milioni 2.4 kati ya tani milioni 3.6 zinazozalishwa sawa na asilimia 60 ya uzalishaji wa zao hilo nchini. Kwa wastani zao la ndizi mkoani humo linawaingizia wakulima kati ya shilingi bilioni 240 – 300 kwa mwaka, hivyo kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.
Pia, Dkt. Biteko amesema bado ipo fursa ya kuwekeza kwenye teknolojia na miundombinu ya uchakataji wa zao la ndizi ili kuongeza thamani na kuzalisha bidhaa nyingine zinazotokana na zao la hilo.
“Ninafahamu kwamba, mkoa umebuni na kuanzisha mradi wa Mashamba Makubwa ya Kahawa yenye ukubwa wa ekari 10,000. Mradi ambao unalenga kuwanufaisha watu wapatao 10,000 wakiwemo vijana na utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2024 – 2027. Kwa kuanzia tayari shamba lenye ukubwa wa ekari 400 katika Kijiji cha Makongora wilayani Muleba ambapo kila kijana amegawiwa ekari moja ya shamba lililoandaliwa na kupewa miche bure,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, lengo la mradi huo likitajwa kuwa ni kuongeza ajira kwa vijana, pato la mtu mmoja na pato la mkoa pamoja na kuongeza pato la halmashauri kupitia ushuru wa zao la kahawa na kuliingizia Taifa fedha.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa amesema kuwa Tamasha la Ijuka Omuka (Kumbuka Nyumbani), limelenga kuwakutanisha pamoja wakazi wa Kagera na kuibua fursa za uwekezaji mkoani humo.
Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000