TANZANIA NA JAPAN ZAISAINI MKATABA WA MSAADA WA BILIONI 27.3 KUSAIDIA SEKTA YA AFYA

Dar es Salaam

TANZANIA NA JAPAN ZAISAINI MKATABA WA MSAADA WA BILIONI 27.3 KUSAIDIA SEKTA YA AFYA

Tanzania na Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo (JICA), zimetiliana saini mkataba wa msaada wa Yen za Japan bilioni 1.527 (sawa na shilingi bilioni 27.3) kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya nchini.

Mkataba huo umesainiwa katika Ofisi za Hazina Ndogo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Yoichi Mikami na 

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Bw. Hitoshi Ara, kwa niaba ya Serikali ya Japan.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, alisema kuwa fedha hizo zitatumika katika ununuzi wa vifaa-tiba ili kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto. 

Dkt. Mwamba alisema kuwa, ufadhili huo muhimu unaendana na Mpango wa sasa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao pamoja na masuala mengine, unalenga kutatua changamoto za ubora katika utoaji huduma za afya nchini. 

“Ufadhili huu unaunga mkono juhudi za Serikali kwenye sekta ya afya, zinazolenga kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wakati kwenye jamii,” alisema Dkt Mwamba.

Aliongeza kuwa mradi huo utatekelezwa na Wizara ya Afya na utaboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma bora za afya hususani Huduma ya Mama na Mtoto kwa kuwa na vifaa-tiba vya kisasa vitakavyoongeza uwezo wa kufanya uchunguzi na matibabu katika Hospitali saba za Rufaa ambazo ni: Dodoma, Tumbi iliyoko mkoa wa Pwani, Mount Meru iliyoko Arusha, Sekou-Toure iliyoko Mwanza, Songea iliyoko Ruvuma, Maweni iliyoko mkoani Kigoma na Hospitali ya Lumumba iliyoko Zanzibar.

“Msaada huu ni mwendelezo wa ushirikiano unaokua kati ya nchi zetu mbili kama inavyodhihirishwa na kuongezeka kwa idadi ya miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia misaada na mikopo nafuu”

Dkt Mwamba aliishukuru Japan kwa ufadhili huo na mingine ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kuchochea maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi na kuboresha Maisha ya Watanzania. 

“Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo kwa faida ya watu wetu na Serikali itachukua hatua zote muhimu kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa” alisema Dkt. 

Mwamba.

Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini, Mhe. Yoichi Mikami, alisema kuwa kwa kutambua ushirikiano wa nchi hizo mbili, Japan imekuwa ikitoa misaada katika sekta ya afya ili kuchochea maendeleo ya watanzania. 

“Serikali ya Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuchochea maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi na kuboresha Maisha ya Watanzania,” alisema Mikami.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Bw. Hitoshi Ara, alisema kuwa JICA imekuwa ikitoa msaada mkubwa katika sekta ya afya ya Tanzania kwa miaka mingi, katika kuimarisha usimamizi wa hospitali na kujenga uwezo wa usimamizi wa ubora wa huduma za afya kupitia mbinu mbalimbali, katika Hospitali za Rufaa za Kanda. 

Bw. Hitoshi alisema kuwa, JICA wamekuwa wakishuhudia maboresho katika ufanisi, usalama, na ubora wa huduma na wanamini kuwa hayo yote yamechangia kwa kiasi kikubwa katika kufikia lengo la Mpango was Upatikanaji wa Huduma za Afya kwa Wote (Universal Health Coverage (UHC)) nchini Tanzania.

Aliongeza kuwa wakati viwango vya vifo vya kina mama nchini Tanzania vimeimarika kwa kiasi kikubwa, kutoka 760 kwa kila vizazi 100,000 mwaka 2000 hadi 238 mwaka 2020, pia vifo vya watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano vimepungua.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Bw. Ismail Rumatila, alishukuru kwa msaada huo na alisema kuwa utasaidia kununua vifaa katika hospitali saba za rufaa vitakavyoongeza uwezo mkubwa wa uchunguzi na matibabu.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000