TANZANIA KUENDELEA KUWA NCHI YA KUTEGEMEWA KATIKA KUKUZA USHIRIKIANO :RAIS DKT SAMIA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwa nchi ya kutegemewa katika kukuza ushirikiano wa kimataifa, kuchochea ukuaji wa kiuchumi, na kudumisha amani na usalama barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Rais Dkt, Samia ameyasema hayo wakati wa hafla maalum aliyoiandaa kwa ajili ya Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yaliyopo nchini.
Hafla hiyo huandaliwa kila mwanzo wa mwaka kutakiana heri, kuzungumzia maendeleo nchini na kueleza vipaumbele vya Tanzania ikiwemo kikanda na kimataifa.
Pamoja na mambo mengine, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa pamoja na kuadhimisha miaka 60 ya Muungano, mwaka 2024 Tanzania ilishuhudia ukuaji wa kiuchumi wa asilimia 5.4 ambao umechagizwa na kukua kwa uzalishaji, uwekezaji na utalii.
Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa nchi ilipiga hatua za kihistoria katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya reli na nishati inayoenda kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini Tanzania.
Aidha, Rais Dkt. Samia amebainisha kuwa mwaka 2025 Tanzania itakamilisha maandalizi ya Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa na mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje; nyaraka zitakazobainisha vipaumbele vya nchi na zitakazoongoza pia ushirikiano kati ya Tanzania na wabia wake.
Kimataifa, Tanzania inakusudia kuendelea kuimarisha mahusiano na wabia wake na kukuza mahusiano kwenye sekta muhimu za maendeleo ikiwemo elimu, afya na nishati.
Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000