TANZANIA IPO TAYARI KUPOKEA WAKUU WA NCHI  AFRIKA KATIKA MKUTANO WA NISHATI WA MISSION 300 -DKT.KAZUNGU

Abu Dhabi, UAE

▪️Aliambia Jukwaa la IRENA UAE kuwa Tanzania imejipanga vema kwa ujio huo.

▪️Asema Tanzania imerekehisha sheria ya uwekezaji kuruhusu  sekta binafsi kutekeleza miradi

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia umeme na nishati jadidifu Dkt Khatibu Kazungu amesema ,Tanzania imejipanga vema kupokea ugeni wa Wakuu wa Nchi 53 wa Afrika watakaohudhuria mkutao wa wakuu wa nchi wa masuala ya nishati  unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 hadi 28 Januari, 2025 jijini Dar es Salaam.

Dkt Kazungu ameyasema hayo kwenye mkutano wa Baraza la 15 la wakala wa kimataifa wa nishati jadidifu (IRENA) wakati akiwasilisha mada kwenye mjadala wa ngazi ya juu wa Mawaziri wenye lengo la kujadili namna ambavyo nchi wanachama wanaweza kutumia fursa ya ushawishi kwa wadau wa maendeleo kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya nishati jadidifu ambayo ni rafiki kwa mazingira

‘’ Nipende kuwajulisha kuwa Tanzania ni mwenyeji wa mkutano huo wa masuala ya nishati  na ajenda hii kama nchi tumeibeba kwa vitendo kuhakikisha waafrika Milioni 300 kusini mwa jangwa la Sahara wanapata umeme ifikapo mwaka 2030 na natoa rai kwa  nchi wanachama wa IRENA kuibeba ajenda hii kwa vitendo.‘’ Amesema Dkt. Kazungu

Amesema  mkutano wa M300 utaangazia pia mageuzi kwenye sekta ya nishati na kuangalia uwezekano wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuunganisha wateja sambamba na ushirikishwaji wa sekta binafsi kwenye utekelezaji wa miradi ya pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia

Aidha Dkt. Kazungu amewaambia wajumbe wa IRENA kuwa kauli mbiu itakayoongoza mkutano huo ni kuharakisha upatikanaji wa nishati Afrika ili kuwatoa gizani waafrika wapatao milioni 685 kati ya Bilioni 1 ambao hawana nishati ya umeme

Dkt Kazungu amesisitiza kuwa Serikali imefanya marekebisho ya sheria ya uwekezaji ili kutoa fursa kwa sekta binafsi kushirikiana na Serikali kutekeleza miradi ya nishati jadidifu kutokana na umuhimu wake

Amesema Tanzania inawashukuru sana wabia wa maendeleo kwenye utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu kama vile Benki ya Dunia, Benki ya maendeleo ya Afrika AfDB, AFD, KFW kwa kufadhili miradi mbalimbali ya nishati jadidifu nchini ikiwemo ule wa Kakono na Malagarasi ambayo iko kwenye hatua za utekelezaji

Kwa upande  Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Nishati na Mabadiliko ya Tabia Nchi kutoka Benki ya AfDB,  ambao pia wanafadhili miradi ya nishati jadidiifu kwa upande wa Afrika Kevin Kariuki alisema kuwa utashi wa kisiasa, uainishaji wa sera za wazi vinahitajika sana kwenye utekelezaji wa miradi ya umeme kwa nchi za Afrika ili iweze kuleta tija kwa wananchi wake

Alisema ni wakati sasa kwa nchi za Afrika  kuchangamkia fursa za utekelezaji wa miradi ya nishati ambayo ni rafiki kwa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza hewa ya ukaa na kuzitaka jumuiya za kimataifa kuunga mkono azimio hilo kwa vitendo.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000