SEKTA YA NISHATI IPO SALAMA CHINI YA RAIS SAMIA – DKT. BITEKO

📍Urambo, Tabora 

▪️Akagua Kituo cha Kupoza umeme – Urambo

▪️Amshukuru mama Sitta kwa mchango wake katika mradi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya umeme huku akisisitiza kuwa ni lazima  Watanzania wapate huduma ya umeme.

“ Tunamshukuru Mhe. Rais ambaye anasema wananchi wapate umeme, Naomba nikuahidi Mhe. Rais mimi na wenzangu tutafanya kazi kwa kasi unayohitaji ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme” amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko amesema hayo Mei 2, 2025 wilayani Urambo, mkoani Tabora mara baada ya kukikagua Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha Msongo wa Kilovoti 132/33.

Dkt. Biteko amelipongeza na kulishukuru Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kukamilisha mradi kwa ufanisi “ Mmefanya kazi kwa vitendo, nilikuja hapa mwaka jana mradi ukiwa asilimia 10, maajabu gani mmefanya mmemaliza kazi kwa wakati siwezi kujua. Nataka niwaambie naona fahari kuwa kiongozi wenu, napenda kufanya kazi na watu wenye kuleta matokeo nawashukuru mno,”

Vilevile, ameipongeza Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme ( ETDCO) kwa usimamizi mzuri wa Kituo hicho cha Urambo  ambacho kimewashwa kwa siku 20 hadi sasa na kuongeza mapato ya TANESCO kwa asilimia 10.

Ameitaka Kampuni hiyo kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kusema kuwa wana fursa ya kupewa mradi mwingine kwa kuwa wamefanya kazi nzuri.

Amewahakikishia wananchi wa Urambo na Kaliua kuwa wataendelea kupata umeme wa uhakika na mradi huo unaifanya Tabora kuwa chanzo cha umeme katika mikoa ya Katavi na Kigoma.

Amesisitiza “ Mwisho wa  mwezi huu wa tano tutazima jenereta Mpanda na kusaidia  wao wapate umeme, watu wa Urambo nataka niwaambie kabla ya Kituo hiki kuwashwa makusanyo ya TANESCO yalikuwa milioni 323 pekee na baada ya kuwashwa Wilaya ya Urambo inaweza kuipatia TANESCO kwa mwaka shilingi bilioni 4.5 kiuchumi maana yake tumewekeza shilingi bilioni 44 na hiyo fedha itarudi ndani ya muda mfupi,”

Sambamba na hayo, Dkt. Biteko amempongeza Mbunge wa Urambo, Mhe. Margaret Sitta kwa mchango wake na ufuatiliaji wa ujenzi wa mradi wa Kituo hicho na kusema kuwa alijitoa kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya umeme.

Aidha, amesema sekta ya nishati imenufaika na mchango wake na kuielekeza TANESCO kupanda mti na kuupa ukumbi wa mikutano jina la Mbunge huyo ikiwa ni sehemu ya kuthamini na kuenzi mchango wake.

Pia, ameielekeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupeleka umeme katika vitongoji huku Urambo ikipewa kipaumbele.

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025, amewasihi Watanzania kushindana kwa hoja na sera, huku akiwaomba wamuunge mkono Rais Samia kwa nia yake thabiti ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Mbunge wa Jimbo la Urambo, Mhe. Margaret  Sitta amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 wamepata fedha zaidi ya shilingi bilioni 100 ambapo barabara imetumia shilingi bilioni 12, sekta ya elimu imetumia shilingi bilioni 25 pia wana shilingi bilioni 7 kwa ajili ya ujenzi wa matanki ya maji huku wakisubiri mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria.

Kuhusu umeme, Mhe. Sitta amesema awali wananchi  walikuwa wakichanga fedha kwa ajili ya kununua jenereta lakini sasa wanaishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa umeme.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kufuatia maelekezo na usimamizi makini wa Dkt. Biteko sasa wananchi wanapata umeme wa uhakika.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000