RAIS SAMIA APELEKA NEEMA MKOANI TANGA

Tanga 

▪️Bilioni 20 kusambaza umeme katika vitongoji 180

▪️Zaidi ya Kaya 5,940 kufikiwa

▪️RC Tanga amshukuru Rais Samia, awasisitiza wananchi kuchangamkia fursa

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatekeleza mradi wa Shilingi Bilioni 20 wa kusambaza umeme katika vitongoji 180 utakaonufaisha zaidi ya Kaya 5,940 Mkoani Tanga.

Hayo yameelezwa na Meneja Usimamizi wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Romanus Lwena akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy Mei 22, 2025  wakati wa kumtambulisha Mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi, Kampuni ya Transpower Limited na International Contractor Limited Jv kwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian.

“Leo hii tupo hapa Mkoani Tanga kwa ajili ya kumtambulisha mkandarasi ambaye atatekeleza mradi huu wenye thamani ya shilingi 20,581,548,011.20,” alibainisha Mha. Lwena.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea mradi huo ambao alisema unakwenda kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi wake na alimsisitiza mkandarasi kuhakikisha anatoa ajira kwa wananchi wa maeneo ya mradi.

“Wananchi wa Tanga tujitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa, mradi unaotekelezwa ni mkubwa hivyo mbali na manufaa tutakayopata baada ya kukamilika kwa mradi lakini pia kuna fursa nyingi wakati wote wa hatua zote za utekelezaji wake ikiwemo ajira na biashara mbalimbali,” alisisitiza Mhe Dkt. Burian.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi, Mhandisi Lwena alisema mradi unatekelezwa katika majimbo 12 ya uchaguzi na kwamba kwa kila jimbo vitongoji 15 vitafikiwa na mradi.

Alitaja majimbo ambayo ni Jimbo la Tanga, Pangani, Mkinga, Muheza, Korogwe Mjini, Korogwe Vijijini, Lushoto, Bumbuli, Mlalo, Handeni Mjini, Handeni Vijijini na Kilindi.

Alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme ambapo alibainisha kuwa gharama ya kuunganisha umeme kupitia mradi huo ni shilingi 27,000 pekee.

“Katika mradi huu, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ruzuku ili kila mwananchi aweze kuunganisha umeme kwa gharama ya shilingi 27,000, tumuunge mkono kwa kuchangamkia fursa hii,” alisisitiza Mha. Lwena.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkandarasi kutoka Kampuni ya Transpower Ltd, Mha. Cuthbert Shirima alisema kampuni hiyo inao uzoefu wa muda mrefu na aliahidi kufanya kazi kwa weledi na kukamilisha mradi huo kwa kipindi cha miezi 18 badala ya 24 iliyoainishwa katika mkataba.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000