RAIS MWINYI NA WANANCHI WA UKONGORONI
*RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mambo mengi na kuboresha sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuleta mageuzi makubwa kwenye miundombinu ya Afya, Elimu na Maji safi.*
Amesema ujenzi wa skuli na hospitali za ghorofa kwa Wilaya zote za Unguja na Pemba na majimbo yote ya Zanzibar kuenea skuli za kisasa, kuimarishwa kwa miundombinu ya maji safi kwa ujenzi wa matangi ya maji na kuenezwa visima ili kuwaondoshea wananchi adha ya huduma za jamii sambamba na ujenzi wa barabara zenye kiwango cha lami.
Alhajj Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye Ibada ya Sala ya Ijumaa na dua maalumu aliyoandaliwa na wananchi wa wazee wa Vijiji vya Ukongoroni na Charawe ikiwa ni sehemu ya shukurani yao baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Ukongoroni hadi Charawe pamoja na kuipongeza Serikali kwa hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa kwenye kukuza huduma za jamii nchini.
Akizungumzia ujenzi wa Hospitali ya Binguni ambayo ni ya Rufaa ,Mkoa wa Kusini Unguja, amesema tayari fedha za ujenzi zimepatikana.
Aidha, Alhajj Dk. Mwinyi amewaahidi wananchi wa Mkoa huo Ujenzi wa barabara ya Tunguuu hadi Makunduchi kwa mwendelezo wa barabara hiyo iliyoishia Tunguu.
Alisema, Serikali imeazimia kujenga njia mbili kulia na kushoto na taa za barabarani chini ya kampuni ya Brazil, aidha Alhajj Dk. Mwinyi ameridhia ombi la wananchi wa Chwaka kujengewa daraja kwenye barabara ya Chwaka.
Pia, Alhajj Dk. Mwinyi aliwashukuru wananchi kwa Mkoa wa kusini Unguja kwa shukurani zao na dua ya kuombea maendeleo makubwa kwa Serikali yao.
Sambamba na hilo pia aliwaasa waumini na wananchi wa Mkoa huo kuenedela kuliombea taifa kwa mambo makubwa mawili ikiwemo kuendelea watu kuishi kwa amani na mshikamano pamoja na kuendelea kuwaombea dua viongozi kwa kuyatekeleza yote waliyowaahidi.
Nae Mbunge wa jimbo hilo akatoa shukrani kwa Rais Dk.Mwinyi na Serikali anayoiongoza.
Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000