POLISI ARUSHA INAWASAKA WALIOHUSIKA NA WIZI NDANI YA GARI.
Jeshi la polisi Mkoa wa Arusha linaendelea kufanya uchunguzi pamoja na kuwatafuta wale wote waliohusika kwenye tukio la wizi ndani ya gari aina ya Toyata Alphard yenye namba za usajili T. 340 EJR kama ilionekana kwenye mitandao ya kijamii kupitia picha mjongeo.
Leo Januari 14, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo mnamo Januari 12, 2025 maeneo ya Kaloleni Jijini Arusha ambapo inadaiwa mwanaume mmoja aitwaye Goodluck Matingisa (41) anadai kuibiwa mali zake.
Kamanda Masejo amesema kuwa bado Jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na taarifa zaidi zitatolewa.
Aidha, Kamanda Masejo ametoa wito kwa wananchi kuachana na tabia ya kubeba vitu vya thamani na kutembea navyo ndani ya magari bila ya kuwa na ulinzi wakati wa kuyaacha maeneo ya maegesho.
Sambamba na hilo SACP Justine Masejo amewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu ili hatua za kisheria ziendelee kuchukuliwa.
Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000