MIL.600/- KUKAMILISHA KITUO CHA AFYA UKUMBI-KILOLO

Kilolo

Naibu Waziri wa Afya, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange, amesema serikali itatoa sh. milioni 600 kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya cha kisasa katika Kata ya Ukumbi, Wilaya ya Kilolo.

Dkt. Dugange ametoa kauli hiyo alipokutana na wananchi wa kata hiyo katika mkutano wa hadhara wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya sekta ya afya na elimu wilayani humo.

 Amepongeza juhudi za wananchi kwa kutenga ekari 13 za ardhi na kuchangia sh.milioni 45 kwaajili ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kitaboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa zaidi ya wakazi 14,000.

“Serikali italeta si chini ya milioni 600 ili kukamilisha kituo cha afya cha kisasa chenye majengo yote muhimu, TAMISEMI tunataka ujenzi ukamilike na huduma za awali zianze kutolewa kwa wananchi ifikapo Machi 30, 2025,”amesema.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Mhe. Justin Nyamoga, amesema wananchi walijitoa kujenga kituo hicho baada ya zahanati waliyoitegemea kuwekwa kwenye eneo la barabara na kutarajiwa kubomolewa.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Dkt. Clemance Konkamkula, ujenzi wa kituo hicho ulianza mwaka 2011 kwa mapato ya ndani ya halmashauri, ambapo jengo la wagonjwa wa nje (OPD) limefikia asilimia 75 kwa gharama ya sh. milioni 132.

Halmashauri inahitaji sh. milioni 850 kukamilisha mradi, ikiwemo ujenzi wa wodi mbili, jengo la maabara, jengo la upasuaji, nyumba za watumishi, jengo la mionzi, na majengo mengine muhimu kwa utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wa Kata ya Ukumbi.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000