MHE. MCHENGERWA: RUFAA 5,589 ZA WAGOMBEA ZIMEKUBALIWA
Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kati ya rufaa 16,309 za wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa zilipokelewa, rufaa 5,589 zimekubaliwa.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dodoma Novemba 16, 2024, Waziri Mchengerwa amesema rufaa hizo ni pamoja na zilizowasilishwa baada ya muda wa nyongeza wa siku mbili na uamuzi wake umezingatia dosari ambazo zilisababisha kutoteuliwa kwao awali hazikuwa kubwa zinazoathiri matokeo yaliyokusudiwa na kanuni.
Aidha, amesema katika nafasi zinazogombewa vyama 18 vya siasa vimeweka wagombea katika nafasi 30,977 kati ya nafasi 80,430 sawa na asilimia 38.51 huku Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiweka wagombea katika nafasi zote.
Amesema katika nafasi za mwenyekiti wa kijiji zinazogombewa ni 12,280 ambapo vyama hivyo vimeweka wagombea katika nafasi 6,060 sawa na asilimia 49.35.
Pia, amesema nafasi za mwenyekiti wa mtaa zinazogombewa ni 4,264, vyama viliweka wagombea katika nafasi 3,281 sawa na asilimia 76.94 na nafasi za mwenyekiti wa kitongoji zinazogombewa ni 63,886 vyama vimeweka wagombea 21,636 sawa na asilimia 33.87.
Hata hivyo, ametaja baadhi ya sababu zilizosababisha wengine kutoteuliwa ni kukosa sifa ya uraia watanzania, kujidhamini wenyewe, kutojiandikisha kwenye daftari la wapigakura wa serikali za mitaa na wengine kuwa chini ya umri wa miaka 21.
Pamoja na hayo, amesema Ofisi ya Rais – TAMISEMI imefuatilia tuhuma zilizotolewa kwenye maeneo mbalimbali na kubaini hazikuwa na ukweli na zililenga kuleta taharuki na kuchafua mchakato wa uchaguzi unaoendelea vizuri.
Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000