MHE. CHANDE AWATAKA WATAALAM KUJIKITA KATIKA TAFITI ZITAKAZOTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI
Arusha
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), amewataka wataalam nchini kuendelea kufanya tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Mhe. Chande aliyasema hayo katika Mahafali ya Ishirini na Sita ya Chuo cha Uhasibu Arusha, yaliyofanyika katika Ukumbi wa TTC katika Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Mhe. Chande alisema kuwa ufanyaji wa Tafiti hizo utasaidia jamii na Serikali kubaini maeneo yenye changamoto na kuyafanyia kazi ili kujenga ustawi wa maisha bora kwa wananchi na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa jumla.
‘’Napenda kutoa rai kwa wataalamu wetu kuendelea kufanya tafiti zitakazosaidia jamii na Serikali kubaini maeneo yenye changamoto, ili muweze kushauri ipasavyo Serikali na taasisi nyingine za elimu ya juu’’ alisema Mhe. Chande.
Mhe. Chande aliongeza kuwa ili na wataalam mahiri nchini, Taasisi za elimu ya juu zinatakiwa kuanzisha mitaala inayoendana na mahitaji ya wakati kwenye soko la ajira kwa Sekta ya Umma na Binafsi, ambapo aliutaka uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha kuendeleza sifa njema iliyojiwekea ya kuzalisha wataalam mahiri na wenye weledi ambao wanakubalika katika soko la ajira.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Profesa Eliamani, Sedoyeka, alisema kuwa pamoja na utoaji wa mafunzo Chuo kimeendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za Serikali ikiwa ni pamoja na majeshi ya hapa nchini ikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi.
’Kupitia ushirikiano huu, wapo wa wahitimu wetu wa kwanza wa Shahada ya Uzamili ya Usalama wa Taarifa (Master of Information Security) kutoka Shule ya Polisi Tanzania ambao ni matunda ya ushirikiano kati ya jeshi hilo na Chuo cha IAA. Alisema Prof. Sedoyeka.
Awali, akizungumza katika Mahafali hiyo Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Dkt. Mwamini Tulli, alisema Mahafali ya 26 ya Chuo hicho ni sehemu ya mafanikio na matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na wafanyakazi na Menejimenti ya Chuo cha Uhasibu Arusha.
Dkt. Tulli aliupongeza Uongozi wa Chuo kwa namna wanavyojituma katika kuhakikisha Chuo kinakua na kufikia malengo na mipango mbalimbali waliyojiwekea katika utoaji wa mafunzo, kufanya tafiti na utoaji wa ushauri wa kitaalam nchini.
‘’Kwa namna ya kipekee nawapongeza sana watumishi wa Chuo cha IAA kwa namna walivyojituma kufanikisha mahafali hii, wamepambana vya kutosha” Alisisitiza
Mahafali ya 26 ya Chuo cha Uhasibu Arusha yamejumuisha wahitimu 5,854 katika ngazi za astashahada, stashahada, shahada na shahada za uzamili ambapo kati ya wahitimu hao wanaume ni 3601 na wanawake ni 2,253.
Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000