MBUNGE MAVUNDE AKABIDHI MATOFALI 41,000 NA SARUJI TANI 102 KUCHOCHEA SHUGHULI ZA MAENDELEO DODOMA JIJI

Dodoma

▪️Ni kuunga mkono miradi inayoibuliwa na wananchi kwa kata zote 41

▪️Jiji la Dodoma latenga Bilioni 6 kuunga mkono miradi inayoibuliwa na wananchi

▪️Vifaa kulenga kuboresha sekta ya Afya na Elimu

Mwenyekiti wa kamati ya Mfuko wa kuchochea maendeleo ya Jimbo na Mbunge wa Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde leo amekabidhi matofali 41,000 na Saruji tani 102 kwa kata zote 41 za Dodoma Mjini kwa lengo la kuunga mkono miradi inayoibuliwa na wananchi katika ujenzi wa miundombinu ya Elimu na vituo vya Afya.

“Mfuko wa Jimbo hujielekeza katika miradi ya kipaumbele ya Elimu,Afya na uwezeshwaji wananchi kiuchumi.

Leo tunakabidhi matofali na saruji kwa kata zote 41 kwa lengo la kuunga mkono miradi inayoibuliwa na wananchi.

Kwasasa Jiji la Dodoma limetenga Shilingi Bilioni 6 kuunga mkono miradi yote inayoibuliwa na wananchi ili kuchochea maendeleo zaidi ndani ya Dodoma Jiji.

Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan amefanya kazi kubwa sana ya kuiendeleza Dodoma hivyo ni wajibu kazi hii nzuri kuungwa mkono kwa wivu mkubwa”Alisema Mavunde

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mh. Jabir Shekimweri na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Dodoma Ndg. Charles Mamba wamepongeza hatua ya Mfuko wa Jimbo kujibu mahitaji ya jamii na hasa katika kuboresha sekta ya Elimu na Afya na hivyo kusaidia kusogeza maendeleo kwa wananchi kwa ukaribu zaidi.

Akitoa taarifa ya mfuko wa Jimbo,Mratibu wa Mfuko Bi. Debora Muwinje amesema mfuko wa Jimbo la Dodoma Mjini unapokea kiasi cha Shilingi Milioni 93 kuchochea maendeleo kiasi ambacho kimetumika na kugharamia mahitaji ya vifaa husika na kumpongeza Mbunge Mavunde kwa kuchangia mifuko ya saruji 1000 ya ziada ili kuhakikisha eneo kubwa zaidi linaguswa.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000