MAKAMU WA RAIS ATEMBELEA KITUO CHA UMAHIRI CHA MATIBABU CHA AFRIKA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amepongeza uwepo wa kituo cha Umahiri cha Matibabu cha Afrika (AMCE) ambacho amesema kitakua mfano kwa bara la Afrika na kusaidia kuokoa gharama kupeleka wagonjwa nje ya bara hilo.
Makamu wa Rais amesema hayo alipotembelea Kituo cha Umahiri cha Matibabu ya Kibingwa cha Afrika kilichopo Abuja nchini Nigeria. Amesema kituo hicho kitasaidia kuhamisha maarifa na hivyo kuwezesha wazawa kuweza kutoa huduma za afya endelevu kwa wananchi wa Afrika.
Amewapongeza wataalamu ambao walihudumu katika hospitali mbalimbali nje ya Afrika kwa uamuzi wao wa kurejea barani Afrika na kushirikiana na wazawa katika kutoa huduma hospitalini hapo.
Makamu wa Rais ameshuhudia uwepo wa vifaa tiba vya kisasa na mashine mbalimbali za upimaji na matibabu ambazo zitasaidia kutoa huduma za kibingwa zilizoshindwa kupatikana kwa muda mrefu.

Kituo hicho ambacho kimefadhiliwa na Benki ya Afrexim kimewekwa miundombinu na vifaa tiba vya kisasa kwaajili ya matibabu ya kibingwa kukabiliana na maradhi mbalimbali ikiwemo saratani.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Rais wa Benki ya Afrexim Prof. Benedict Okey Oramah, mazungumzo yaliyofanyika kando ya Mkutano wa 32 wa Benki ya Afrexim unaofanyika Abuja nchini Nigeria.
Pamoja na mambo mengine, mazungumzo hayo yamelenga kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Benki ya Afrexim hususani katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati.
Makamu wa Rais yupo nchini Nigeria kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 32 wa Benki ya Afrexim unaofanyika Jijini Abuja.







Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000