KATIBU MKUU NDUNGURU ASISITIZA  MATUMIZI YA MFUMO WA BENKI MTANDAONI KATIKA AKAUNTI ZA VITUO VYA AFYA MSINGI 

Dodoma

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Adolf Ndunguru, amefungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa Benki mtandaoni (Internet Banking) kwa akaunti za vituo vya kutolea huduma za afya msingi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya mfumo huo Machi 13, 2025 yaliyofanyika jijini Dodoma, Ndunguru amesisitiza kuwa mfumo huo utaimarisha uwazi, ufanisi na usalama wa fedha za umma kwa kuondoa matumizi ya hundi katika akaunti za serikali.

Amesema mafunzo hayo yanaenda sambamba na maboresho ya Mfumo wa Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS), unaolenga kuhakikisha kuwa vituo vyote vya kutolea huduma vinafanya malipo kwa njia ya kielektroniki.

“Mfumo huo umeanza kutumika katika akaunti mbili za mpango wa m-mama tangu mwishoni mwa mwaka wa fedha 2023/24, na unatarajiwa kupanuliwa kwa hospitali za wilaya kuanzia Mei 2025, huku vituo vingine vikijiunga kuanzia Julai 2025,”amesema.

Amesema Benki ya NMB imeonesha ushirikiano mkubwa katika mchakato huo ikiwa na zaidi ya akaunti 40,846 zinazotumika kwenye vituo vya kutolea huduma. Aidha, benki nyingine kama CRDB, NBC na DCB pia zimeanza kutoa huduma za Internet Banking kwa akaunti za Serikali.

 Katibu Mkuu Ndunguru ametoa wito kwa benki zote zinazohudumia akaunti za vituo vya kutolea huduma kushirikiana na serikali kuhakikisha kuwa mafunzo hayo yanafanikiwa na mfumo huo unatekelezwa kikamilifu kwa manufaa ya wananchi.Mafunzo haya yamehudhuriwa na Maofisa wa TAMISEMI, wakuu wa vitengo, Wawekahazina wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, pamoja na wadau wa sekta ya benki

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000