KASEKENYA ASISITIZA MAFUNZO KWA WATUMISHI
Singida
![](https://admin-k.kigogomedia.com/app/uploads/2025/02/GjrGmRVXcAEGs6K.jpeg)
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya ameitaka Menejimenti ya Wizara ya Ujenzi, kuhakikisha inaandaa programu nzuri za mafunzo kwa watumishi wa Wizara hiyo ili kuwaendeleza na kuwajengea uwezo katika utendaji wao wa kazi.
Kasekenya ametoa agizo hilo, mkoani Singida, wakati akifunga mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo ambapo amesisitiza kuwa ni muhimu kwa watumishi kupata mafunzo ili kuendana na kasi ya mabadilko ya teknolojia.
“Viongozi hakikisheni mnaandaa mafunzo kwa watumishi wenu, sio mfanyakazi ana miaka kumi au zaidi hajawahi kupata mafunzo, ili kupata utendaji bora kazini ni muhimu watumishi kupatiwa mafunzo kwani Teknolojia inabadilika kila siku”, amesema Kasekenya.
Aidha, Kasekenya amesisitiza Viongozi kutenda haki kwa wafanyakazi wanaowasimamia na kutoa Motisha ili kusaidia kupunguza msongo wa mawazo na ukali wa maisha.
![](https://admin-k.kigogomedia.com/app/uploads/2025/02/GjrGmRbXQAEa69b.jpeg)
Amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo mbalimbali anayoyatoa kwa Wizara ya Ujenzi ambayo yamesaidia uimarishaji wa miundombinu katika Sekta ya Ujenzi ikiwemo ujenzi na utengenezaji wa barabara, madaraja, vivuko na ujenzi wa viwanja vya ndege.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde amesema kuwa Baraza hilo limepata fursa ya kujadili kwa kina masuala mbalimbali ya kiwizara na kupata elimu ya afya ya akili ili kudhibiti msongo wa mawazo.
Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Sekta ya Ujenzi umefanyika mkoani Singida ambapo ajenda kuu katika Mkutano huo ni kupokea, kujadili na kuidhinisha Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2025/26 kabla ya Bajeti hiyo kuwasilishwa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushirikisha wajumbe mbalimbali kutoka Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara.
![](https://admin-k.kigogomedia.com/app/uploads/2025/02/GjrGmRWWwAAqFuG.jpeg)
![](https://admin-k.kigogomedia.com/app/uploads/2025/02/GjrGnSeW0AA5-tO.jpeg)
![](https://admin-k.kigogomedia.com/app/uploads/2025/02/GjrGnSWXYAA-qGd.jpeg)
![](https://admin-k.kigogomedia.com/app/uploads/2025/02/GjrGnSeW8AA9cSN.jpeg)
![](https://admin-k.kigogomedia.com/app/uploads/2025/02/GjrGnSeW8AA9cSN-1.jpeg)
Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000