“CHATO MSIFANYE MAKOSA KUCHAGUA VYAMA VINGINE,”-DKT. BITEKO

Chato,Geita

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza wananchi wa Chato kuchagua wagombea wa CCM ili kuendeleza miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya yao.

Dkt. Biteko amesema hayo  Novemba 23,2024 wakati akihutubia katika  Kampeni zinazoendelea za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Wilaya ya Chato zilizofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Bwanga, vilivyopo mkoani Geita. 

Amesema CCM ina nia ya kuendelea kuleta maendeleo huku  akivitaka vyama vingine vishindane kwa hoja sio kwa matusi na kuwa nyenzo za kuunganisha  Watanzania sio kuwagawa.

“ Nawaomba muwasikilize vyama vingine lakini msifanye kosa la kuwachagua maana wanataka vyeo tu, msikubali watu wanaowaambia mkunje ngumi hawana ilani iliyopitishwa na wananchi wala bajeti wanataka muwachague wakafanye kazi gani?,” amehoji Dkt. Biteko.

Ameendelea kusema Uchaguzi wa Mwaka 2024,  CCM imejipanga kushinda na si kubahatisha kwa kuwa na mipango yake imeanza kwa wanachama wake kujitokeza kwenye uandikishaji daftari la wapiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“ Chato waliojiandikisha kwenye daftari la kupiga kura walifika zaidi ya 200,000 na  bila shaka wataenda kupiga  kura, CCM tuna uwezo wa kuleta maendeleo kwenye wilaya yenu, viongozi watakaochaguliwa wataenda kufanya kazi kwa sababu ilani ipo, CCM wana ilani na mipango wengine hawana,” ameeleza Dkt. Biteko.

Aidha, amesema tangu Rais Samia aingie madarakani CCM imekuwa na kauli mbiu ya kazi iendelee huku ikiendeleza kwa juhudi kubwa miradi ya maendeleo kwa maslahi ya nchi .

Ametaja miradi hiyo  kuwa ni mradi wa kufua wa umeme wa  Bwawa la Julius Nyerere ambao sasa unafanya kazi, treni ya umeme ya kisasa (SGR) inafanya kazi kutoka Dar es salaam hadi Dodoma, kuimarisha shirika la ndege kwa kuongeza idadi ya ndege.

Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amesema CCM inaheshimu Uchaguzi huo wa Serikali Mtaa na ndio maana viongozi wake wote wamesambaa katika  maeneo mbalimbali kueleza umuhimu wa uchaguzi huo.

“ CCM tuna sababu za kuomba kura kwa sababu tumepiga kazi na inaoonekana watu wa Chato tupigie kura kuchagua wagombea wa CCM katika vitongoji vyote na vijiji hakuna kumwachia mtu kwa kuwa wengine hawana ilani wala mipango,” amefafanua Dkt. Biteko.

Mbunge wa Chato, Mhe. Dkt. Medard Kalemani ametoa shukrani kwa Rais Samia kwa jitihada zake za kuiletea maendeleo wilayani Chato.

Amebainisha  katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Chato imepata shilingi bilioni 197.28 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo. “Tumepata shilingi milioni 100 kwa ajili ya kujenga kituo cha mabasi, kwenye kituo cha afya Rais Samia ametupa fedha kwa ajili ya kukikarabati,”

Amesisitiza “ Hapa Bwanga awali kulikuwa na shida ya umeme tunakushukuru sasa umeme umefika katika vitongoji na vijiji 15. Nataka nikuhakikishie kwa fedha tulizopata za miradi mikubwa kumi ikiwemo mradi wa uwanja wa ndege ambao unaendelea vizuri ndege zinatua, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mipango na Fedha kimekamilika na mwezi ujao kinafunguliwa, ujenzi wa maktaba ya kanda inayogharimu shilingi bilioni 7.2 ambayo imeshaezekwa,” 

Amewahimiza wananchi wa Bwanga kuchagua wagombea wa CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuendeleza  maendeleo Bwanga na Chato kwa ujumla

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000