RAIS SAMIA ASHIRIKI MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA NACTE NA KUTOA AGIZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameiagiza
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano
na Teknolojia ya Habari kuendelea kufunga mtandao katika vijiji vyenye umeme ili
kuwawezesha wanafunzi kufanya mitihani ya masomo ya sayansi kwa mtandao.


Rais Samia ametoa maagizo hayo leo wakati wa hafla ya kilele cha Maadhimisho ya
Miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) iliyofanyika katika Ofisi za Baraza hilo.


Aidha, Rais Samia amesema serikali imefanya uwekezaji kwenye TEHAMA ambao
umeimarisha utendaji wa Baraza na kuongeza matumizi ya teknolojia katika usajili wa
watahiniwa, uchapaji na usahihishaji wa mitihani na uchakataji wa matokeo.


Rais Samia pia amesema Serikali itaendelea kuijengea uwezo NECTA na walimu ili
kuhakikisha ufundishaji, usomeshaji na utahini unafanyika kwa umahiri mkubwa
kuwawezesha watahiniwa kumudu mahitaji ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.


Vile vile, Rais Samia ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na
NECTA kutafuta mkakati wa kushughulikia changamoto ya udanganyifu wa mitihani.
Aidha, Rais Samia pia amelitaka Baraza la Mitihani kuhakikisha wanatekeleza
majukumu yao kuendana na shabaha ya sera ya elimu hususan katika upimaji wa
umahiri.


Rais Samia amesema serikali itaendelea kuimarisha utendaji wa Baraza kulingana na
mazingira mapya ya kiteknolojia na kushirikiana na Baraza hilo ili lifikie malengo ya
muda mrefu ya kuweka mitambo ya kisasa ya uchapaji kadri uwezo utakavyoruhusu.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000