MHE. KAIRUKI AZINDUA MKAKATI WA UTEKELEZAJI WA SERA YA WANYAMAPORI NA MPANGO WA USIMAMIZI WA TEMBO

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amezindua Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Wanyamapori 2023 – 2033 na Mpango wa usimamizi wa Tembo Tanzania 2033 – 2033, lengo ikiwa ni kukabiliana na changamoto mbalimbali za Uhifadhi wa Wanyamapori. Uzinduzi huo umefanyika usiku wa Desemba 15, 2023 katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

Amesema uzinduzi wa mkakati huo, ni mwendelezo wa mikakati ya Serikali ya kulinda rasilimali za Wanyamapori ambapo Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuweka mazingira ya kisera, kuimarisha mfumo wa kisheria na udhibiti wa uhifadhi, ulinzi, usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali za Wanyamapori.

Aidha, amesema mkakati huo utatekelezwa kwa kuzingatia matumizi ya sayansi na teknolojia katika kukabiliana na changamoto za uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori.

Katika hatua nyingine, ili kuongeza vyanzo vya mapato, Mhe. Kairuki amesema Serikali kwa kushirikiana na Wadau imeandaa Mpango wa Ufadhili na Ukusanyaji Fedha (2023 -2033) kupitia Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Wanyamapori ili kukusanya rasilimali zinazohitajika.

Hafla hiyo imehudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo, mabalozi kadhaa, asasi za kimataifa za mazingira Watumishi na Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na kupambwa na bendi ya msanii maarufu Mrisho Mpoto.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000