MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR AMUWAKILISHA DKT SAMIA KWENYE MAADHIMISHO YA MIAKA 15 YA JUWAUZA.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025, imeweka Sera na Mikakati mbali mbali pamoja na kuchukua hatua za kuwawezesha watu wenye ulemavu kuweza kukamilisha malengo yao na kuweza kutoa mchango katika kuliendesha Taifa.

Ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan katika kufunga Maadhimisho ya Miaka kumi na Tano (15)ya Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA) uliofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip uwanja wa ndege Zanzibar.

Mhe. Rais Dkt Samia amesema kwa kutambua mchango mkubwa unaotolewa na watu wenye Ulemavu Serikali imeweza kutoa nafasi za uongozi kwa watu wenye ulemavu katika Wizara mbali mbali nchini ambapo wanaendelea kufanya vizuri katika majuku yao siku hadi siku.

Amesema kuwa Serikali imeanzisha Mabaraza ya Watu wenye Ulemavu kwa wilaya zote za Unguja na Pemba ambayo yanasaidi upatikanaji wa ujumuishwaji wa masuala ya watu wenye Ulemavu katika Taasisi zote za Umma na kuleta haki na fursa za watu wenye ulemavu nchini.

Aidha Serikali imeanzisha Mfumo wa Maendeleo ya watu wenye Ulemavu ambao katika mwaka wa fedha 2023-2024, Serikali imetenga Bajeti ya Shilingi milioni mia mbili(200, 000,000) kwa lengo la kuwanufaisha watu wenye Ulemavu kujiendeleza Kiuchumi.

Sambamba na hayo Rais Dkt Samia amesema Serikali inaendelea kutoa Mikopo kwa wajasiriamali na kwa kuweka kipaumbele kwa watu wenye Ulemavu kupitia fedha za ahueni ya UVIKO 19, fedha za mapato yatokanayo na Serikali pamoja na Mfuko wa Khalifa Foundation Fund kupitia wakala wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar.

Amefahamisha kuwa Serikali imejenga Skuli mbili (2) za Dahalia kwa watu wenye Ulemavu Unguja na Pemba kwa lengo la kuhakikisha watu wenye Uemavu wanaendelea kupata fursa sawa za elimu kama watu wengine sambamba na kutunga Sheria ya watu wenye Ulemavu Nam.(8) ya mwaka 2022 kwa lengo la kuwalinda na kutetea haki na fursa za watu wenye Ulemavu wakiwemo wanawake.

Dkt Samia amesema Serikali imekuwa ikiwawezesha watu wenye ulemavu kushiriki katika mashindano ya Kimataifa yaliyofanyika katika nchi mbali mbali Duniani sambamba na kushiriki katika Warsha iliyoshirikisha Mataifa Kumi na Tano(15) yenye lengo la kutoa Mafunzo na kutayarisha wataalamu wa Michezo Jumuishi itakayowajumuisha watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu bila ya kuwa na Utengano wa aina yoyote.

Rais Dkt Samia ametoa wito kwa Taasisi za Serikali, Sekta binafsi na washirika wa Maendeleo kuiunga mkono JUWAUZA na Taasisi nyengine za watu wenye Ulemavu pamoja na kuitaka jamii kuendelea kutoa mashirikiano kwa watu wenye Ulemavu ili waweze kushiriki katika Ujenzi wa Taifa.

Mapema kaimu waziri wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratib na Baraza la Wawakilishi Mhe. Hamza Hassan Juma amesema JUWAUZA ni Taasisi ya kupigiwa mfano na kuigwa kwa namna wanavyoisaidia Serikali katika kupambania haki za wanawake na wasichanya wenye ulemavu Zanzibar kwa kuona kuwa wanathaminiwa na kupewa kipaumbele katika shuhli mbali mbali za Kimaendeleo.

Amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuthamini michango inaotolewa na Jumuiya ya JUWAUZA na kuahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendela kushirikiana nao katika kufikia adhma na malengo ya jumuiya hio yanafikiwa.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar Ndugu Abdulwakil Haji Hafidh amesema JUWAUZA Inasimamia haki za wanawake na wasichana wenye Ulemavu kwa kuwapatia elimu, ushirikishwaji katika mambo mbali mbali ya kijamii, kiuchumi na Kisiasa.

Unataka kutuma habari? Submit on tuma kwetu kupitia info@kigogomedia.com au WhatsApp 07000000